TFF imejibu hoja zote zilizoandikwa
na gazeti la Nipashe la May 8 2017 juu ya tuhuma mbalimbali, kwa mujibu ya
Saiti ya TFF tunakuletea yalioandikwa kwenye saiti hiyo.
Gazeti la Nipashe limekuwa
likichapisha makala maalum katika matoleo yake ya kuanzia tarehe 8 Mei 2017
yakituhumu Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kujihusisha na ‘ufisadi
wa kutisha’.
Gazeti hili limekuwa likitumia
maulizo ya kiukaguzi (audit queries) yaliyoibuliwa na wakaguzi wa fedha wa TAC
miaka mitatu iliyopita, ambayo hata hivyo tayari yalikwishapatiwa majibu, na
kuandika vichwa vya habari vinavyolituhumu shirikisho kujihusisha na ‘ufisadi
wa kutisha’. Baadhi ya querry hizi zinahusiana na malipo/marejesho ya miaka ya
2002/03 enzi za FAT.
Wakaguzi wa mahesabu baada ya kufanya
kazi yao waliandaa management report ambayo iliibua queries au maswali kuhusu
matumizi mbalimbali ya fedha. TFF ilijibu maulizo (queries) hayo kwa ufasaha na
taarifa kufikishwa mbele ya mkutano mkuu ambao ulipokea na kukubali majibu
hayo.
Hata hivyo gazeti la Nipashe
limekuwa likitoa taarifa ya upande mmoja tu ambayo ni ya kupotosha, haina
ukweli na inakiuka misingi mitatu ya uandishi wa habari ambayo ni usahihi wa
habari (accuracy), kusikiliza pande zote (balance) na kutenda haki na kutoa
uzito sawa kwa pande zinazohusika kwenye habari (fairness).
TFF imekuwa ikitafakari dhumuni hasa
la chombo hiki kikubwa cha habari kuamua kukiuka misingi hii na kuanza
kuporomosha tuhuma nzito kwa viongozi wa TFF bila kuwapa nafasi ya kusikilizwa
au hata kuomba majibu yatokanayo na audit queries za wakaguzi wa TAC.
Mwenendo huu wa gazeti la Nipashe wa
kukiuka maadili kwa makusudi kipindi hiki muhimu katika historia ya soka
Tanzania, unalenga kudhoofisha juhudi za TFF na serikali za kuwahamasisha
wananchi kuichangia timu yao ya vijana inayoshiriki mashindano ya mataifa ya
Afrika kule Gabon, na pia unalenga kushawishi uchaguzi mkuu wa shirikisho
utakaofanyika miezi mitatu ijayo.
Hata hivyo, shirikisho limeona
inafaa kutoa ufafanuzi kwa kifupi wa masuala yaliyopotoshwa kwenye magazeti ya
Nipashe kwa faida ya wasomaji na wapenzi wa mpira wa miguuu kwa ujumla:-
1.
Mamilioni ya Coca-Cola:
Baada ya kupokea audit queries, marejesho
yalifuatiliwa na yalipatikana.
2.
Madai ya kuwalipa wadai mbalimbali kama Punchline, Atriums, Michael
Wambura, n.k.
Ieleweke kuwa TFF ni taasisi
endelevu, hivyo uongozi mpya unapoingia madarakani unapokea mali na madeni
(assets and liabilities). Na baada ya kuingia madarakani mwezi Novemba, 2013
uongozi ulikumbana na kadhia ya kupokea vitisho vya mali zake kukamatwa
kutokana na malimbikizo ya madeni mbalimbali. Kuna kipindi mali na akaunti za
TFF zilikamatwa na madalali wa mahakama kwa nia ya kuziuza kufidia madeni
tuliyokuta na ikabidi tuzikomboe ili warejeshewe hasa pale ambapo TFF inakuwa
haina pesa kabisa na timu za taifa zinakuwa na mahitaji kama usafiri na kulipia
kambi. Viongozi wa TFF hawawezi kukubali timu za taifa zisisafiri kisa TFF
haina pesa.
Hivyo TFF ilichukua jukumu la kulipa
madeni hayo licha ya kuwa na majukumu mengine ya kuendesha timu za taifa na
shughuli nyingine za kiutawala na maendeleo ya mpira wa miguu kwa ujumla.
Baada ya kulipa madeni hayo,
kulitolewa maelezo ya kina baada ya kupokea audit queries. Lakini pia ieleweke
kuwa uendeshaji wa mpira unahusisha mahitaji mengi ya fedha mengine ya dharura
na ikitokea hivyo watu hutoa fedha zao mfukoni ili warejeshewe baadaye.
3.
Kuhamia mjini:
Maamuzi ya kuhamia ofisi mpya kwenye
jengo ya PPF yalifanyika na kubalikiwa na Kamati ya Utendaji. TFF ina mamlaka
chini ya katiba yake kuhamisha ofisi ndani ya mkoa bila kuomba ridhaa ya Kamati
ya Utendaji. Kwa hiyo, halikuwa wazo wala maamuzi ya mtu mmoja bali ilikuwa ni
pendekezo lililopitishwa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
TFF ilihamishia ofisi mjini ili kuwa
katika mazingira mazuri zaidi ya utendaji na kuboresha mawasiliano.
Na kuhama huko kwa muda kulifanyika
wakati ofisi za TFF zinakarabatiwa. Ilikuwa ni kupisha mradi wa uendelezaji wa
Uwanja wa Karume.
PPF ni Shirika la Umma ambalo wakati
huo kulingana na ushindani wa kupata ofisi mjini ilionekana kuwa nafasi ya kukidhi
mahitaji ya TFF.
Kwa hali ya mahitaji ya “Corporate
World” hasa kwa kuangalia dunia ya kisasa za uendeshaji mpira unaotegemea corporate world kwa vyo
vyote ile iko siku TFF itahamia mjini na Ofisi za Uwanja wa Karume kubakia ni
Technical Center kama ilivyo kwa nchi kama Zimbabwe, Afrika Kusini, Senegal
nakadhalika.
4.
Ukwepaji kodi:
TFF imekuwa ikilipa kodi zake zote
na imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na TRA kuhakikishia hakuna
malimbikizo. Kuna suala la kodi za kabla ya mwaka 2013 ambalo pamoja na
mazungumzo na serikali kuendelea bado TFF imekuwa ikiendelea kulipunguza na mpaka
sasa imelipa zaidi ya shilingi bilioni moja ndani ya miaka mitatu.
5.
Mikataba ya manunuzi na ukarabati wa jengo:
Manunuzi ya TFF yanatokea kadiri
mahitaji yanavyojitokeza na upatikanaji wa fedha. Na ieleweke kuwa TFF ni
taasisi isiyo ya kiserikali na haibanwi na sheria ya manunuzi iliyotungwa na
Bunge. Na manunuzi mengine yanafanyika kwa kutumia fedha za FIFA ambazo
mrejesho wake unakuwa wa kuridhisha ndio maana mpaka sasa FIFA waniamini TFF.
6.
Kutokuwepo na mkaguzi wa mahesabu wa ndani:
Suala la kuwa na mkaguzi wa ndani ni
muhimu katika taasisi yoyote lakini vilevile taasisi inaweza kuwa na muundo
ambao una udhibiti sawasawa na ukaguzi wa ndani. Hata hivyo inahitaji maamuzi
ya kamati ya utendaji ili kuweza kubadilisha muundo wa shirikisho (Organization
Chart). Na siku zote kamati ya utendaji huyafanyia kazi maoni ya wakaguzi na
kuyatekeleza kutegemea mahitaji na wakati.
7.
Kutumia interns kufanya kazi:
TFF inaamini katika kuwapa vijana
nafasi na hata kuwapa uzoefu wale wanaotoka vyuoni.Kila mwaka TFF hupokea
vijana kutoka mashuleni na vyuoni ambao miongoni mwao wamekuja kuwa watumishi
wa kuajiriwa baada ya masomo yao. TFF itaendelea kuwapa uzoefu vijana katika
kada mbalimbali huku wakisimamiwa na viongozi wazoefu walio ndani ya
shirikisho.
8.
Ajira ya Edgar Masoud (RIP):
Upo uthibitisho wa muhtasari wa
Kamati ya Utendaji unaoonyesha kuwa utaratibu wa ajira ya aliyekuwa Mkurugenzi
wa Fedha, hayati Edgar Masoud na kusitishwa ajira yake ulifuata taratibu zote
ikiwa ni pamoja na maamuzi ya kawaida kupitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF.
9.
Mkutano na Waandishi wa Habari:
Kama Rais wa TFF, anaweza kufanya
mkutano na wanahabari yaani press conferences nje ya Karume. Nyingi huwa
tunafanyia nje ya ofisi kulingana na mahitaji vikiwa vikao vya Kamati ya
Utendaji na kamati mbalimbali.
10.Ukarabati:
Ukarabati huu ulifanyika kwa fedha
za FIFA, kanuni za FIFA zinasoma hivi matumizi ya chini ya dola 50,000
hayahitaji zabuni/tenda. Isitoshe FIFA walileta pesa ili kazi ifanyike. Kazi
hii ilifanyika taratibu na pole pole kwa kiasi TFF iloivyokuwa inapata pesa.
Huu utaratibu uko mpaka leo.
11.Tuhuma kuhusu matumizi ya fedha
za wafadhili (sponsors):
TFF imekuwa ikivutia wafadhili
mbalimbali kuwekeza katika TFF. TFF huwa inaandaa program zake na ratiba kwa
kutegemea fedha za ufadhili. Lakini mara nyingi ipokeaji wa fedha za ufadhili
umekuwa ukichelewa na kukuta program mbalimbali zilikwiaanza/kumalizika. Ili
kutokwamisha program mbalimbali TFF huwa ina utaratibu wa kutumia pesa toka
vyanzo mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya program na kurudisha pesa hizo wakati
wafadhili wakilipa. Vyanzo hivi ni pamoja na kutumia pesa za ruzuku/wafadhili
wengine/kuazimwa pesa kwa muda mfupi. Huu utaratibu ni muda mrefu kuanzia miaka
ya tisini hadi sasa.
Utaratibu huu umekuwa ukitumiwa kwa
sababu shughuli za mpira zinatokea katika mazingira ya dharura na lazima
zifanyike. Kama kuna mechi za kucheza za timu ya taifa na mfadhili hajatoa
pesa, lazima TFF ikope kutoka vyanzo vingine ikiwemo watu binafsi, kama
viongozi wa shirikisho na mashirika ili kuhakikisha taifa halipati adhabu kwa
kutoshiriki mashindano husika au kufanya maandalizi yanayotakiwa.
Tunapenda kuviasa vyombo vya habari
kufanya kazi yao kwa weledi. Ushabiki au kuandika habari kwa kupotosha
kutaathiri mpira wa miguu Tanzania. Kutawakatisha tamaa mashabiki na
kuwakimbiza wadhamini. Uchaguzi unapita lakini, mustakabali wa taifa unabaki
palepale. Uweledi uwepo katika kuripoti kwa lengo la maendeleo ya mpira wa
miguu
Chanzo http://www.tff.or.tz/news/872-taarifa-za-uongo-na-uzushi-zinazochapishwa-na-nipashe
0 Comment untuk "Isome hapa Taarifa nzima ya TFF dhidi ya tuhuma za ufisadi zinazoenezwa na gazeti la Nipashe"