Kocha Mkuu wa timu ya Mpira wa
Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Mayanga amemwongeza Kiugo wa Young
Africans, Emmanuel Martin kwenye kikosi chake kinachojindaa kucheza na Botswana
Jumamosi Septemba 2, mwaka huu.
Mchezo huo wa kirafiki wa
kimataifa utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam chini ya
utaratibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Emmanuel Martin anatarajiwa
kujiunga na kambi ya Taifa Stars mara moja leo Agosti 30, mwaka huu na kuanza
na mazoezi na wenzake yatakayofanyika jioni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es
Salaam.
Emmanuel Martin ameongezwa na
Mayanga baada ya mawasiliano kuonesha kwamba huenda akawakosa nyota wa
kimataifa Simon Msuva kutoka Difaa El Jadidah ya Morocco na Orgenes Mollel wa
FC Famalicao ya Ureno.
Taarifa kutoka Morocco inaonesha
kwamba Msuva ana kibali cha muda cha kuingia na kutoka Morocco ‘visa’ ambacho
kinamnyima haki ya kutoka na kuingia Morocco mara kwa mara.
Kuna juhudi zinafanywa na timu
yake kadhalika Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco kumfanikishia kupata
kibali cha muda mrefu ili iwe rahisi kwa mchezaji kutoka na kuingia kama
anahitaji katika timu ya taifa.
Kuhusu Mollel taratibu za ruhusa
za kimataifa zinafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria za nchi ya Ureno ambako
anacheza soka la kulipwa.
Nyota wengine wote wameripoti
Taifa Stars wakiwamo wale wa kutoka nje ya mipaka ya Tanzania kama vile Mbwana
Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Elias Maguli (Dhofar FC/Oman), Abdi Banda (Baroka
FC/Afrika Kusini), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya) wakati Farid Mussa wa CD
Tenerif ya Hispania anatarajiwa kutua leo.
Wengine ambao wako kambini Hoteli
ya Sea Scape iliyoko Kunduchi, Dar es Salaam ni makipa Aishi Manula (Simba SC),
Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Young Africans).
Pia wamo Walinzi ni Gadiel
Michael (Young Africans), Boniphas Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young
Africans), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).
Viungo ni Himid Mao - Nahodha
Msaidizi (Azam FC), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Shiza
Kichuya (Simba SC), wakati Washambuliaji ni Raphael Daud (Young Africans) na
Kelvin Sabato (Azam FC).
Benchi la Ufundi la Mayanga
linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha
Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt.
Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na
Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).
C&P from TFF site
Millionaire Ads
0 Comment untuk "Emmanuel Martin aitwa Stars kuchukua nafasi ya Simoni Msuva"